Jaji Mkuu Martha Koome amewahakikishia Wakenya kuwa Idara ya Mahakama itasalia huru na bila upendeleo katika kusikiliza na kuamua mizozo ya uchaguzi ya mwaka 2027.
Akizungumza na Wanahabari Jumatano tarehe 28 Oktoba 2026, Koome amesema mahakama hazitahusishwa katika mashindano ya kisiasa, akisisitiza kuwa kesi zote zitashughulikiwa kwa haki, kwa kuzingatia ushahidi na sheria.
“Ninataka kuwahakikishia Wakenya kuwa Idara ya Mahakama haitahusishwa katika mashindano ya kisiasa kwa sababu sisi si wanasiasa, bali ni majaji na maafisa wa mahakama,” amesema Koome.
Katika kujiandaa kwa uchaguzi huo, Idara ya Mahakama imeanzisha mpango wa mafunzo unaolenga zaidi ya majaji, maafisa wa mahakama na wafanyakazi wengine 400, kupitia Chuo cha Mahakama cha Kenya na Kamati ya Mahakama kuhusu Uchaguzi.
Mafunzo hayo yanalenga kuimarisha uwezo wa mahakama kusikiliza na kuamua mizozo ya uchaguzi kwa ufanisi, kwa kuzingatia muda uliowekwa kisheria.
Koome amesema maandalizi hayo pia yanahusisha kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na ushahidi wa kidijitali na matumizi ya teknolojia katika uchaguzi.
Aidha, amesema Idara ya Mahakama inaimarisha mifumo ya usimamizi wa kesi, utunzaji wa kumbukumbu na upangaji wa vikao ili kupunguza ucheleweshaji wa kesi za uchaguzi.
“Mizozo ya uchaguzi lazima isuluhishwe ndani ya muda madhubuti uliowekwa na sheria,” amesema Koome.
Jaji Koome pia amewataka viongozi wa kisiasa, vyama, wagombea na wafuasi wao kuheshimu uhuru wa mahakama na kuruhusu kesi kuendelea bila vitisho au shinikizo lisilofaa.
Amesisitiza kuwa tofauti za kisiasa zinapaswa kushughulikiwa kupitia njia halali, huku kila mlalamikaji akipewa haki ya kusikilizwa bila kujali msimamo wake wa kisiasa.
Idara ya Mahakama imesema itaendelea kuimarisha uwezo wa wafanyakazi, miundombinu ya kiteknolojia na rasilimali zinazohitajika kuhakikisha inatekeleza wajibu wake wa kikatiba wakati wa uchaguzi wa 2027.









