Mwanasoroveya Julius Rotich anayetaka kuwa kamishna wa tume huru ya uchaguzi (IEBC) amewalaumu wanasiasa kwa kuwa na tabia ya kuwahonga wapiga kura wakati wa uchaguzi.
Akifika mbele ya jopo linaloendelesha mahojiano ya kuwatafuta makamishna wa IEBC, Rotich amesema njia ya kipekee kutatua hili ni kutoa hamasisho kwa wapiga kura kuzingatia maadili wanapowachagua viongozi.
Rotich amezua gumzo wakati wa mahojiano hayo alipofichua kwamba walikuwa wanahesabu hata mbwa kama wapiga kura wakati wa mfumo wa mlolongo mwaka 1987.
Mhadhiri wa chuo kikuu Dr. Joseph Nganga vile vile amehojiwa ambapo amejijitetea kwa kusema kuwa ana uwezo wa kutatua matatizo yanayotokea wakati wa uchaguzi.
Jopo la uteuzi ambalo linaongozwa na Dr. Elizabeth Muli limemhoji pia Juliana Cherera ambaye ametakiwa kujibu maswali mbalimbali ambayo yanahusiana na mchakato wa uchaguzi.
Hadi kufikia sasa, watu kumi na nane kati ya 36 walioorodheshewa wamehojiwa kwa nafasi hizo ambazo zilisalia wazi kufutia kujiuzulu kwa makamishna wanne.