Mahakama Kuu imetoa uamuzi wa kuzuia kwa muda kuapishwa kwa makamishna wateule wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Katika uamuzi huo, Jaji Lawrence Mugambi amesema ameruhusu Bunge kuendelea na mchakato wa kuwapiga msasa wateule saba wa nyadhifa za mwenyekiti na makamishna.
Hata hivyo, amesema hawataruhusiwa kuapishwa hadi pale kesi ya kupinga mchakato wa uteuzi itakaposkilizwa na kuamuliwa.
“Ombi hili limeibua masuala ya msingi ya kisheria na hivyo nimeliwasilisha kwa Jaji Mkuu Martha Koome ili ateue jopo la majaji kusikiliza kesi hii,” alisema Jaji Mugambi.
Mapema mwezi huu, Rais William Ruto alimpendekeza Erastus Edung Ethekon kuwa mwenyekiti wa IEBC. Pia aliwateua Anne Nderitu, Moses Mukwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor, Francis Odhiambo, na Fahima Abdalla kuwa makamishna.
Hata hivyo, Kelvin Roy Omondi na Boniface Mwangi waliwasilisha kesi mahakamani wakidai kuwa mchakato wa uteuzi haukuzingatia Katiba.
Bunge la Kitaifa, kupitia kiapo chake, lilieleza kuwa ni kwa manufaa ya umma kuwa mchakato wa kuwapiga msasa makamishna hao wateule kupigwa msasa na kuidhinishwa.
“Katiba inalitambua Bunge la Kitaifa kama chombo cha kuthibitisha uteuzi wa watu wote waliopendekezwa kuteuliwa kuwa wanachama wa tume za kikatiba au wamiliki wa ofisi huru,” lilisema Bunge la Kitaifa.
Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula sasa anatarajiwa kutoa mwelekeo kwa Bunge kuhusu hatua zitakazofuata kutokana na uamuzi huo.









