Wakili mmoja ameelekea mahakamani akisaka agizo la kumzuia Rais William Ruto kuajiri washauri Zaidi akisema hakuna kipengee cha sheria kinachoongoza mchakato wa kuajiriwa kwa washauri.
Wakili Vincent Lempaa katika ombi lake mbele ya mahakama ya Milimani, anahoji kuwa ombwe katika sheria imetumiwa visivyo na Rais Ruto kuajiri wanasiasa kama washauri ambao wameongeza gharama kwa mlipa ushuru.
Lempaa aidha anataka mahakama kuagiza washauri walioajirwa kwa sasa kutolipwa hadi pale kesi aliyowasilisha itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Rais Ruto kwa sasa anawashauri 21 wengi wao wakiwa wanasiasa walioshindwa kwenye uchaguzi mkuu uliopita na mawaziri na wakuu wa utawala wake waliofutwa kazi.
Washauri wa Ruto ni pamoja na Makau Mutua (Masuala ya Katiba), Moses Kuria (Mshauri wa Uchumi), David Ndii (Mwenyekiti wa Baraza la Rais la Washauri wa Kiuchumi), Monica Juma (Mshauri wa Usalama), Dominic Menjo (Mshauri wa Usalama wa Chakula), Edward Kisiang’ani (Mshauri Mkuu wa Uchumi), na Jaoko Oburu (Mshauri Maalumu wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi).
Wengine ni Silvester Kasuku (Mshauri wa Utawala), Harriette Chiggai (Mshauri wa Haki za Wanawake), Abdi Guliye (Mshauri wa Mifugo na Usimamizi wa Mifugo), Nancy Laibuni (Mjumbe Msaidizi wa Baraza la Washauri wa Uchumi), na Augustine Cheruiyot (Mkuu wa Sekretarieti ya Rais) miongoni mwa wengine









