Baraza la Magavana (CoG) sasa linatishia kuanzisha mchakato wa kumwondoa Mdhibiti wa Bajeti, CPA Margaret Nyakang’o, likimtuhumu kuwa kikwazo kikuu katika utekelezaji mzuri wa majukumu ya serikali za kaunti.
Kwa mujibu wa magavana hao, Nyakang’o ameonyesha tabia ya ukaidi na kutokuwa na mashauriano, wakidai kwamba amekuwa akileta urasimu usio wa lazima ambao umechelewesha upatikanaji wa fedha kwa kaunti—hali wanayosema imevuruga shughuli za kila siku na haiwezi kuvumiliwa tena.
Gavana wa Wajir, FCPA Ahmed Abdullahi, ameonya kuwa Baraza hilo liko tayari kuchukua hatua za kisheria, ikiwemo kuwasilisha ombi bungeni la kumng’atua Nyakang’o, kwa lengo la kukomesha kile alichokitaja kuwa vikwazo vya kifedha ambavyo vimeathiri huduma kwa wananchi na kukwamisha maendeleo mashinani.
Ameeleza hali hiyo kama aina ya hujuma ya kimfumo inayokiuka misingi ya ugatuzi na kuathiri kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mvutano huu mpya kati ya Baraza la Magavana na Ofisi ya Mdhibiti wa Bajeti umetokana na masharti mapya ya utoaji fedha kwa kaunti ambayo kaunti zinapaswa kutimiza kabla ya fedha kupelekwa kwenye akaunti zao.









