Makachero wa kupambana na ugaidi (ATPU) wamemkamata mwanamme mmoja kwa madai ya kujifanya mmoja wao na kumhadaa mkimbizi kutoka Ethiopia Zaidi ya shilingi milioni tatu akidai atamsaidia kusajili kama mkenya.
Kwa mujibu wa idara ya upelelezi (DCI), mchungaji Richard Macharia Njuguna anayehusishwa na kanisa la AIPCA huko Juja kaunti ya Kiambu amekamatwa eneo la Ruiru na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Capital Hill, Nairobi.
Inadaiwa kuwa kati ya tarehe 20 Disemba mwaka jana na tarehe 12 mwezi Februari mwaka huu mchungaji Macharia akijifanya kama afisa wa kupamabana na ugaidi alimhadaa mkimbizi huyo fedha hizo.
Upekuzi nyumbani mwa mshukiwa kumepelekea kupatikana kwa stakabadhi na mhuri za taasisi tofauti za serikali ikiwemo za hakimu wa Nairobi, wizara ya ardhi, ubalozi wa Kenya nchini Somalia miongoni mwa nyingine.









