Swala la mabadiliko ya tabia nchi ni la dharura na linahitaji kuangaziwa kikamilifu mara moja.
Haya ni kwa mujibu wa Rais William Ruto ambaye amesema mkutano wa COP 28 mwaka jana jijini Dubai ulibainisha haja ya kuweka mikakati mwafaka ili kupata suluhisho la kudumu kuhusiana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi.
Rais Ruto amesadiki kwamba mkutano wa COP 28 ulionyesha ni wakati kila mmoja kuchukulia swala la mabadiliko ya tabia nchi kama linalohitaji kuangaziwa vilivyo kama vile usalama na amani.
Akizungumza katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (UNEA 6) eneo la Gigiri hapa jijini Nairobi, kiongozi wa taifa amekariri kuwa kwa sasa ni dhahiri shayiri kwamba binadamu wanachingia pakubwa katika kuzorota kwa mazingira.
Akitaja madhara ya mabadiliko ya tabia nchi kwa mfano kiwango cha juu cha joto, ukame, mafuriko maeneo tofauti ulimwenguni, Rais Ruto ametaja sayansi imebainisha kuwa binadamu amesalia kuwa chanzo kikuu cha kubadilika kwa hali ya anga.
Kiongozi wa taifa amezidi kuongeza iwapo hali itaendelea hivyo, basi hakuna budi ila na kuzidi kushudia madhara kwa kiwango cha juu katika siku za usoni
Na katika umahiri wake, amri jeshi mkuu amewalika wajumbe katika mkutano huo kuzuru maeneo tofauti humu nchini likiwemo bunge la nyani huko Naivasha.
Mkutano huo wa UNEA 6 ambao ulianza Jumatatu wiki hii unatarajiwa kukamilika hapo kesho