Serikali ya Kenya imetoa sababu zake za kumfurusha raia wa Uturuki Harun Aydin.
Akikanusha madai ya naibu rais William Ruto kwamba Nairobi imeomba msamaha, waziri wa usalama Dr. Fred Matiang’i amesema Uturuki ilikuwa na ufahamu kuhusu kufukuzwa kwa raia wake.
Waziri Matiang’i amesema mataifa jirani yalikuwa yameibua wasiwasi kumhusu Harun Aydin kwa kusafiri akiwa ameandamana na watu wanaodaiwa kuhusika na pesa haramu.
Matiang’i amewaelezea wabunge mjini Mombasa kwamba walikuwa wamearifiwa kwamba raia huyo alikuwa ameondoka nchini Kenya mara mbili pasipokuwa na ushahidi unaonesha alivyoingia nchini Kenya.
Hili anasema liliwalazimu maajenti wa usalama kumkamata na kisha kuwajulisha wenzao wa Uturuki.
Waziri Matiangi ameongeza kwamba nambari za simu ambazo raia huyo aliwapa hazikuwa zake na kwamba hakuwa na cheti kinachomruhusu kufanya kazi humu nchini.
Aydin ambaye alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa waandamane na naibu rais William Ruto kwenye ziara ya kibinafasi iliyokatizwa kuelekea nchini Uganda alikamatwa na maafisa kutoka kitengo cha kupambanana ugaidi.
Ruto na wendani wake wamekuwa wakiishambulia serikali kufuatia hatua hiyo huku wakiisuta kwa kutumia nguvu kumkufuza mwekezekaji aliyekuwa nchini kihalali.