Kila kitu tayari kwa chaguzi ndogo Matungu, Kabuchai, Mudavadi akilia

0

Wananchi wa maeneo bunge ya Matungu na Kabuchai wanaelekea debeni Alhamisi kuwachagua wabunge wao kufuatia vifo vya waliokuwa wabunge Justus Makokha Murunga na James Mukwe Lusweti mtawalio.

Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imeonya kuwa itawachukulia hatua kali za kisheria watakaodhubutu kuwahonga wapiga kura huku chama cha Amani National Congress (ANC) kinachoongozwa na Musalia Mudavadi kikidai kuwepo kwa mipango ya kuiba uchaguzi wa Matungu kwa faida ya chama cha ODM.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC Wafula Chebukati ametoa hakikisho kwamba kila kitu kiko shwari huku wananchi katika maeneo bunge mawili na wadi nne wakielekea debeni kuwachagua viongozi wao.

Akizungumza huko Machakos, Chebukati amewasihi wapiga kura wa eneo hilo kujitokeza kwa wingi ili kushiriki zoezi hilo huku akiwahakikishia usalama wao na kusema zoezi hilo litakuwa huru na wazi.

Yakijiri hayo

Kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi amelalamikia kile anadai ni njama ya kuiba kura katika uchaguzi mdogo wa Matungu.

Mudavadi amedai kuwa baadhi ya wafanyikazi wa kaunti ya Kakamega wanafanya kazi na maafisa wanaosimamia uchaguzi huo kuhitilafiana na matokeo ya mwisho.

Maeneo yanayoshiriki uchaguzi huo ni maeneo bunge ya Matungu na Kabuchai; wadi za London na Hells Gate kaunti ya Nakuru, wadi ya Kiamokama kaunti ya Kisii na ile ya Huruma kaunti ya Uasin Gishu.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here