Kaunti 18 Zatambuliwa Kuwa Hatarini Wizara ya Afya Ikiweka Mikakati Kukabiliana na El Niño.

0
Katibu wa Afya ya Umma Mary Muthoni
Katibu wa Afya ya Umma Mary Muthoni

 

Wizara ya Afya imeanza maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa kushuhudiwa nchini kuanzia mwezi wa Oktoba 2026 hadi Februari 2027 kwa mujibu wa shirika la hali ya anga duniani WMO.

Katibu wa Afya ya Umma Mary Muthoni amesema Wizara ya Afya inaweka mikakati ya kuhakikisha mfumo wa afya nchini unakabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na hali hiyo ya anga.

Kwa mujibu wa Muthoni, maandalizi ya mapema ni muhimu ili kupunguza madhara na kuhakikisha huduma muhimu za afya zinaendelea kutolewa hasa katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na mafuriko.

Muthoni amesema takriban kaunti 18 zimetajwa kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kuathiriwa na madhara ya El Niño.

Kaunti hizo ni Pamoja na Nairobi,Tana River, Kilifi, Lamu, Mombasa, Kwale, Kisumu, Busia, Siaya, Homa Bay na Migori miongoni mwa kaunti zingine

“Kituo cha Kitaifa cha Operesheni za Majanga kimetambua kaunti 18 zilizo katika hatari kubwa ya kukumbwa na mafuriko.” Amesema Muthoni.

Kaunti hizo zina uwezo mkubwa wa kukumbwa na mafuriko, hali ambayo inaweza kusababisha uharibifu wa miundombinu, kutatiza huduma za afya na kuongeza uwezekano wa wananchi kuathiriwa na magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji chafu.

Aidha Muthoni amesema Wizara ya Afya itafanya kikao na wadau Jumatano tarehe 9 Septemba 2026, ili kutathmini kwa kina athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo na kupanga hatua mwafaka za kukabiliana nazo.

Kikao hicho kitawaleta pamoja wadau muhimu katika sekta ya afya na maeneo mengine yanayohusika na usimamizi wa majanga, kwa lengo la kuhakikisha hatua za tahadhari zinawekwa mapema.

Wizara inatarajia kutumia kikao hicho kupitia mipango ya kukabiliana na magonjwa, kuimarisha ufuatiliaji wa hali ya afya katika maeneo yaliyo hatarini na kuweka mikakati ya kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa wakati.

Ufuatiliaji huo utasaidia kubaini mapema dalili za milipuko ya magonjwa na kuwezesha hatua za haraka kuchukuliwa kabla hali haijawa mbaya zaidi.

Kwa mujibu wa Muthoni, mipango hiyo pia inalenga kuhakikisha wananchi wanakingwa dhidi ya madhara yanayoweza kutokea kabla, wakati na baada ya mvua hizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here