Rais William Ruto amesisitiza kuwa serikali yake haitaruhusu tena kampuni zinazowekeza nchini kusafirisha bidhaa ghafi nje ya nchi kwa ajili ya kuongezewa thamani katika mataifa yao.
Akizungumza katika Kongamano la Biashara la AmCham jijini Nairobi, lililowakutanisha wawekezaji kutoka Marekani na mataifa ya Afrika, Rais Ruto amesema kwa muda mrefu Bara la Afrika limekosa kunufaika kikamilifu na uwekezaji kutokana na baadhi ya kampuni kusafirisha bidhaa ghafi hadi katika nchi zao kwa ajili ya usindikaji na kuongeza thamani.
“Tunataka kujenga uhusiano unaotegemea manufaa ya pande zote.”
“Ndio maana ninawaomba mzalishe hapa nchini Kenya, kwa sababu hapa ndipo kuna ubunifu na uvumbuzi.” amesema Rais Ruto
“Jenga makao yako makuu ya kikanda hapa na uitumikie Bara la Afrika ukiwa hapa.” ameongeza.
Rais pia amesema Mswada wa Kukuza Uwekezaji na Mauzo ya Nje wa mwaka 2026, ambao kwa sasa uko Bungeni, unalenga kuimarisha ulinzi na kurahisisha shughuli za wawekezaji nchini.
Amesema mswada huo unapendekeza hatua mbalimbali za kuwalinda wawekezaji, ikiwemo kulinda mali, mitaji na faida, pamoja na kuanzishwa kwa mahakama maalum ya masuala ya uwekezaji.
“Kupitia Mswada wa Kukuza Uwekezaji na Mauzo ya Nje wa mwaka 2026, ambao kwa sasa uko mbele ya Bunge, tunalenga kuimarisha ulinzi na kurahisisha shughuli za uwekezaji.” Ameeleza Rais.
Kwa mujibu wa Rais, takriban kampuni 100 zinazofanya shughuli katika maeneo maalum ya kiuchumi zimebuni ajira 22,000 katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Aidha, kampuni 118 za usindikaji bidhaa kwa ajili ya mauzo ya nje zimezalisha zaidi ya ajira 32,000.
Rais Ruto amesema hatua hizo ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha Kenya inanufaika zaidi kutokana na uwekezaji kwa kuhamasisha uzalishaji, usindikaji na uongezaji thamani wa bidhaa nchini.









