Kampeini za chaguzi ndogo katika maeneo bunge ya Kabuchai na Matungu zimekamilika rasmi hii leo huku wenyeji wakitazamiwa kuelekea debeni kuwachagua wabunge wapya Alhamisi hii.
Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imesema kila kitu kii shwari kabisa kabla ya chaguzi hizo na kuonya kuwa watakaodhubutu kukiuka kanuni za uchaguzi kwa kuendelea na kampeini za kunadi sera zao watachukulia hatua za kisheria.
Huku kampeini za uchaguzi huo zikikamilika, vyama mbalimbali vya kisiasa vimetumia siku ya mwisho kujinadi kila mmoja akielezea matumaini ya kuibuka na ushindi.
Chama cha Amani Amani National Congress (ANC) kimempigia debe muwaniaji wake wa kiti cha ubunge cha Matungu Oscar Nabulindo katika eneo la Ekama.
Chama hicho kinachoongozwa na Musalia Mudavadi kimeelezea matumaini yake kwamba Nabulindo atachaguliwa mbunge kwenye uchaguzi huo.
Nao wendani wa naibu rais Wiliam Ruto wakiongozwa mbunge wa Malindi Aisha Jumwa wamezuru eneo la Matungu ambapo wamempigia debe Alex Lanya muwaniaji wa kiti hicho kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA).
Naye kinara wa chama cha Ford Kenya Moses Wetangula amempigia debe muwaniaji wa kiti cha ubunge cha Kabuchai Joseph Majimbo Kalasinga.
Vyiti vya Matungu na Kabuchai vilisalia wazi kufuatia vifo vya waliokuwa wabunge Justus Murunga na James Lusweti mtawalia.
Katika uchaguzi wa Matungu, kinyanganyiro ni kati ya Peter Nabulindo wa ANC, David Were wa ODM, Alex Lanya wa UDA, muwaniaji huru Bernard Wakoli miongoni mwa wengine.
Uchaguzi wa Kabuchai, Matungu sawia na wadi za London na Hells Gate kaunti ya Nakuru, Kiamokama kaunti ya Kisii na Huruma kaunti ya Uasin Gishu utafanyika siku ya Alhamisi wiki hii.









