Chama tawala cha Jubilee kimemuandikia msajili wa vyama vya kisiasa kikitaka kuvunja ndoa ya kisiasa baina yake na chama cha PDR kilichobadili jina na sasa kinaitwa UDA.
Jubilee kupitia barua iliyotumwa kwa msajili wa vyama vya kisiasa na katibu mkuu Raphael Tuju kinahoji kwamba UDA kinachohusishwa na naibu rais William Ruto kimevunja maelewano yaliyoafiwa kwenye mkataba wa 2018.
Tuju anahoji kwamba maafisa wa UDA waliohusika kwenye majadiliano ya kubuni ushirikiano huo wa kisiasa wamebadilishwa na sasa chama hicho kina maafisa wapya ambao wamekuwa wakiidhinisha ushindano wa kisiasa katika chaguzi mbalimbali kinyume na makubaliano ya awali.
Jubilee kwenye barua hiyo vile kimelalamikia matumizi ya neno ‘Huslers’ kikisema linakinzana na kauli mbinu yake ya ‘Tuko Pamoja’.
Itakumbukwa kwamba Ruto amenukuliwa akisema kwamba yeye pamoja na wendani wake watahamia UDA iwapo wataendelea kuonewa ndani ya chama cha Jubilee.