Mkenya Faith Cherotich aliandikisha rekodi mpya kwenye mbio za 3000m kuruka viunzi na maji kwenye mashindano ya riadha za dunia za mwaka 2025 jijini Tokyo nchini Japan siku ya Jumatano.
Cherotich mwenye umri wa miaka 21 alimpiku mshindani mkuu wa mbio hizo Winfred Yavi wa Bahrain na kumaliza wa kwanza kwa muda wa 8:51.59.
Yavi, mzaliwa wa Kenya alitwaa nishani ya fedha kwa kumaliza wa pili kwa muda wa 8:56.46, nayo shaba ikitwaliwa na Sembo Almayew wa Ethioipa aliyetimuka kwa muda bora wa kibinafsi wa 8:58.86.
Ushindi wa Cherotich ulifuatiwa na Reynold Cheruiyot aliyemaliza wa tatu kwenye fainali za 1500m upande wa wanaume kwa muda wa 3:34.25 na kulifanya taifa la Kenya kuwa na nishani saba kwa jumla katika siku ya tano ya mashindano hayo, nne za dhahabu, moja ya fedha na mbili za shaba nyuma ya Marekani.









