Mahakama yapinga Oparanya kuondolewa kesi ya ufisadi.

0
Waziri wa vyama vya ushirika na biashara ndogo ndogo Wycliffe Oparanya (awali)

Mahakama imepinga uamuzi wa ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (ODPP) wa kumwondolea mashtaka ya ufisadi waziri wa vyama vya ushirika na biashara ndogo ndogo Wycliffe Oparanya.

Hakimu wa mahakama ya Milimani Benjamin Musyoki siku ya Jumanne alifutilia mbali agizo la ODPP la tarehe 8 Julai 2024 la kumwondolea Oparanya kesi hiyo inayohusishwa na kipindi alichohudumu akiwa gavana wa kaunti ya Kakamega akilitaja kuwa kinyume na sheria.

Oparanya alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya mgongano wa kimaslahi, matumizi mabaya ya ofisi, utakatishaji wa fedha na kushiriki njama ya kufanya ufisadi kwa nia ya kujinufaisha na shilingi milioni 56 kinyume na sheria kwa ushirikiano na kampuni mbalimbali zilizokuwa zimepewa zabuni na serikali ya kaunti.

Kulingana na mahakama, ofisi ya ODPP iliingilia majukumu ya tume ya maadili na kukabili ufisadi (EACC) kwa kuruhusu ushahidi mpya kutoka kwa wakili wa Oparanya bila kufanyiwa ukaguzi.

“Uamuzi huo ulikuwa wa kisiri na hivyo basi ulienda kinyume na maslahi ya umma, na kwa hivyo ulihujumu kifungu cha 157(11) cha Katiba,” alisema jaji.

Uamuzi huo ulitokana na ombi la kikatiba lililowasilishwa na mwanaharakati Fredrick Mulaa, aliyedai kuwa uteuzi wa Oparanya kuwa waziri ulikuwa na dosari kwa kuwa alikuwa na mashtaka ya ufisadi ambayo yaliondolewa ghafla.

Kutokana na uamuzi huo wa mahakama EACC sasa ina fursa nyingine ya kupendekeza mashtaka upya dhidi ya Oparanya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here