Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko ameagizwa kufika mahakamani Alhamisi hii wakati wa kutajwa kwa kesi ambapo ameshtakiwa kwa ukora.
Hakimu wa mahakama ya kupambana na ufisadi Peter Ooko amelazimika kutoa agizo hilo kwa mara nyingine baada ya Sonko kukosa kufika mahakamani Jumanne.
Mawakili wake wakiongozwa na John Khaminwa wameiambia mahakama kuwa lipo agizo lingine linalowazuia Polisi dhidi ya kumhoji au hata kumtoa Sonko hospitalini.
Mahakama vile vile imeambiwa kuwa Sonko anatarajiwa kupelekwa Afrika Kusini kufanyiwa upasuaji kwenye paja lake.
Wakili Khaminwa amehoji kwamba mahakama haistahili kuhitilafiana na utaratibu wa mahakama na kuiomba itaje kesi hiyo kwa muda wa miezi miwili.









