Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko ameachiliwa kwa dhamana ya Sh300, 000 pesa taslimu na mdhamini wa kiasi sawa na hicho baada ya kukanusha mashtaka ya wizi wa kutumia mabavu na kuwashambulia watu na kuwaumiza.
Sonko aliyefikishwa mahakamani kwa ambulensi amekanusha mashtaka dhidi yake mbele ya hakimu mkuu wa mahakama ya Kiambu Stella Atambo.
Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena siku 14 kuanzia leo ambayo ni Februari 23 mwaka huu.
Sonko sasa atasubiri hatma nyingine alasiri hii wakati mahakama ya Kahawa itatoa uamuzi kuhusu kesi ambapo anakabiliwa na mashtaka ya ugaidi.
Polisi wanataka azuiliwe kwa siku 30 zaidi ili kuwaruhusu kukamilisha uchunguzi.
Mapema leo, Sonko alikimbizwa katika hospitali ya Nairobi kupokea matibabu baada ya kulalamikia kuumwa na tumbo akiwa rumande.









