Wahusika katika mzozo wa Sudan wameombwa kutangaza kusitisha mapigano bila masharti.
Rais William Ruto alisema Jeshi la Sudan na Kikosi cha Wanamgambo cha RSF lazima pia wakubali kuwekwa kwa eneo lisilo na wanajeshi litakalo ruhusu upitishaji salama wa msaada wa kibinadamu.
Alisema hatua hiyo itazuia kupoteza maisha, kurahisisha upatikanaji wa huduma za umma na kusaidia upatikanaji suluhu kwa mgogoro huo.
Hii, alidokeza, itapelekea uendelezi wa awamu ya mwisho ya mchakato huo wa kisiasa.
“Hii itaweka msingi wa Sudan yenye amani, utulivu na ustawi.”
Aliyasema hayo siku ya Jumatatu mjini Addis Ababa wakati wa mkutano wa Viongozi wa Nchi na Serikali Nne za IGAD zilizoteuliwa kutatua mgogoro wa Sudan ulioangazia mzozo huo.
Viongozi waliohudhuria ni Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Katibu Mtendaji wa IGAD Workneh Gebeyehu, afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura, Martin Griffiths, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Djibouti Mahamoud Ali Youssouf na wawakilishi kutoka Sudan Kusini na pande zinazozozana.
Rais Ruto, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kundi hilo la IGAD, alitaja hali nchini Sudan kuwa mbaya huku data zikionyesha kuwa zaidi ya watu milioni 2.9 wameyahama makazi yao.
Kwa upande mwingine, idadi ya vifo imefikia zaidi ya 2,000 huku mzozo huo ukitoa shinikizo zaidi kwa nchi jirani.
“Ukubwa wa mgogoro huu wa kibinadamu ni janga la kutisha,” aliuambia mkutano huo.
Huko Darfur, Dkt Ruto aliongeza, mashambulizi yaliyolengwa baina ya makabila yalikuwa yakiongezeka kwa kasi kuelekea mauaji ya halaiki.
“Hali hii ya kutisha inahitaji mazungumzo ya amani ya kijasiri na jumuishi.”