Serikali itawalipia wakenya milioni 1.5 ada ya bima ya afya chini ya mamlaka ya afya ya jamii (SHA) kuanzia wiki ijayo.
Hili ni tangazo lililotolewa na rais William Ruto siku ya Jumanne tarehe 2 Septemba 2025 likilenga wakenya wasio kuwa na uwezo wa kujilipia ada hiyo ambayo Huwa asilimia 2.75 ya mshahara.
“Tofauti na bima ya afya ya awali (NHIF), iliyowalipia wale ambao wangeweza kumudu ada hiyo sawa na waliokuwa wameajiriwa, SHA ni ya kila mkenya. Huduma ya afya si kwa wachache bali ni kwa wakenya wote,” rais alisema.
Akizungumza akiwa katika ikulu jijini Nairobi, rais alisisitiza kwamba serikali ya Kenya hukusanya mapato ya kutosha kugharamia malipo ya wakenya ambao hawana uwezo wa kujilipia bima ya afya.
Kiongozi wa taifa alisisitiza kwamba atakutana na wabunge pamoja na magavana hivi karibuni ili kujadili jinsi idadi hiyo inaweza hata kuongezeka.
Kutokana na hilo amiri jeshi mkuu amewahimiza wakenya kujisajili kwa wingi na mamlaka ya afya ili kuhakikisha kila mmoja anapata huduma bora na nafuu za afya.
Rais ametumia fursa hiyo kuzionya hospitali dhidi ya kuwatoza wagonjwa ada kwa huduma za kutolazwa akisisitiza kuwa huduma hizo zitalipiwa na serikali.









