Kindiki na Wetangula watua Algeria kwa maonyesho ya nne ya biashara ya ndani ya Afrika

0

Naibu Rais Kithure Kindiki na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula wamewasili Algiers, Algeria, kuhudhuria Maonyesho ya Nne ya Biashara ya Ndani ya Nchi za Afrika (IATF).

Kupitia chapisho kwenye ukurasa wake wa X, Wetang’ula amesisitiza kuwa maonyesho hayo yanatoa jukwaa muhimu la kukuza biashara ya ndani ya Afrika na kujenga ushirikiano imara wa kiuchumi.

“Niliwasili Algiers, Algeria, kwa Maonyesho ya Nne ya Biashara ya Ndani ya Afrika pamoja na ujumbe wa Kenya ukiongozwa na Naibu Rais (Prof.) Kithure Kindiki.” Wetangula amesema.

Kulingana na Wetangula, Maonyesho ya 4 ya Biashara ya Ndani ya Afŕika yanalenga kuongeza ufahamu wa uwezekano wa mageuzi wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) kwa mustakabali wa kiuchumi wa Afŕika.

Aidha, sehemu ya mijadala katika maonyesho hayo inatarajiwa kusaidia kutoa mapendekezo ya wazi na ya vitendo ili kuharakisha ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda.

Wetangula amebainisha kuwa sehemu ya maonyesho ya ngazi ya juu ya biashara itakuwepo ambapo inatarajiwa kuzingatia jinsi Afrika inaweza kutumia AfCFTA kufungua uwezo wake kamili wa kiuchumi na kushughulikia vikwazo vya kimuundo na sera.

“Maonyesho hayo yataangazia jinsi Afrika inavyoweza kutumia AfCFTA kufungua uwezo wake kamili wa kiuchumi na kushughulikia vikwazo vya kimuundo na sera ambavyo vitachochea ukuaji wa viwanda, uvumbuzi, na ukuaji jumuishi,” Wetangula alisema.

Maonyesho ya biashara yanayofanyika kila baada ya miaka miwili huleta pamoja serikali, wafanyabiashara, watunga sera, na wawekezaji kutoka barani kote ili kuibua fursa na kuangazia mikakati ya kuharakisha ushirikiano wa kikanda chini ya Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here