Fauka ya Gavana Johnson Sakaja kuepuka shoka la kubanduliwa ofisini baada ya wawakilishi wadi katika bunge la kaunti ya Nairobi kusitisha mpango wao wa kumwondoa madarakani, kamati ya bunge la seneti kuhusu uhasibu wa umma CPAK imemwagiza Sakaja kufika mbele yake.
Kamati hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wake Moses Kajwang inatafta majibu kuhusu matumizi ya fedha katika kaunti ya Nairobi.
Kamati hiyo aidha imeweka masharti makali kufuatia hatua ya baadhi ya magavana kukosa kufika mbele yake akiwemo Gavana Sakaja ikisema kuwa hakuna atakayesazwa katika kuwajibikia matumizi ya fedha za umma.
“Zoezi hili la uwajibikaji ni jukumu letu la kikatiba kwa hivyo ikiwa yeyote atafikiria kuwa atafuata ushauri wa baadhi ya viongozi wetu wa kisiasa kwamba zoezi hili lifanywe katika bunge la kaunti basi utakuwa unajiingiza hatarini. Ikiwa ni pendekezo la kushughulikia uhasibu wa pesa na halijahesabiwa tutatuma faili kwa tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC).”
Kwa mujibu wa Seneta wa Nandi Samson Cherargei sharti Gavana Sakaja afike mbele ya Seneti licha ya kupewa siku 60 kutimiza baadhi ya vigezo ambavyo vilisababisha kutaka kutimuliwa kwake
“Hakuna Magavana walio juu ya sheria. Gavana wa Nairobi bila kujali vita vyake na wawakilishi wadi anapaswa na ni lazima afike mbele ya kamati kujibu kila senti ambayo Jiji la Nairobi imepokea kutoka kwa Wakenya kwa sababu hizo ni pesa za walipa ushuru.”
Haya yanajiri baada ya Rais William Ruto kutangaza kwamba kamati za bunge zimekuwa zikiitisha hongo na kukosa kuwajibika.









