RUTO ATHIBITISHA KIFO CHA POLISI WA KENYA ALIYETOWEKA NCHINI HAITI

0

 

Familia ya Benedict Kabiru, afisa wa polisi wa Kenya ambaye alikuwa ametoweka kwa muda wa miezi sita iliyopita tangu kupotea kwake Mnamo Machi 2025, imetamaushwa na kifo cha mwanao baada ya Rais William Ruto kuthibitisha kifo chake wakati wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA).

Ufichuzi huu unajiri baada ya miezi kadhaa ya serikali kusisitiza kuwa Kabiru yuko hai na bado anafuatiliwa.

Rais Ruto alikiri kuwa afisa huyo aliaga dunia, jambo linalokinzana na matamshi ya awali ya maafisa wa serikali akiwemo Inspekta Jenerali Douglas Kanja ambaye alikanusha ripoti za kifo chake.

Kabiru alitoweka baada ya maafisa wa polisi wa Kenya kuvamiwa na genge moja nchini Haiti.

Familia yake sasa inamtaka Rais Ruto kuratibu juhudi za kurejesha mabaki yake nchini Kenya huku mamaye Kabiru, Jacinta Kabiru, akiikosoa serikali kwa kuwahadaa kwa miezi kadhaa.

“Sasa kwanini wananitesa, kwanini wamenitesa muda wote huku wakijua sana, najua Rais hawezi kutoa taarifa zisizo za kweli, nawaomba walete mabaki ya mwanangu ili nifanye kinachohitajika maana siamini mpaka nione yupo,” alisema mamake Benedict.

Philip Kabiru, kakake Benedict, pia ameikosoa serikali kwa ukimya wake.

“Tulikuamini na mtoto wetu, Benedict. Hivi ndivyo unavyotulipa? Hutupi habari. Huhisi uchungu tunaohisi,” alilalamika Philip.

Familia hiyo tangu wakati huo imeanzisha kesi za kisheria dhidi ya serikali kwa kuficha habari kuhusu jamaa zao, kwa matumaini ya kuwalazimisha maafisa kufichua ukweli.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here