Rais ajaza pengo la mahakama ya upeo

0
Jaji Mohamed Warsame alipokuwa akihojiwa na JSC.

Rais William Ruto amemteua Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mohamed Warsame, kuwa Jaji wa Mahakama ya upeo.

Uteuzi huo ulitangazwa kupitia notisi ya gazeti la serikali ya tarehe 5 Mei 2026.

“Kwa kutumia mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha 166 (1) (b) cha katiba ya Kenya, mimi, William Samoei Ruto, rais wa Jamhuri ya Kenya na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, namteua Jaji Mohamed Abdullahi Warsame kuwa Jaji wa Mahakama ya Juu ya Kenya,” ilieleza notisi hiyo.

Uteuzi huo unafuatia Jaji Warsame kuridhisha Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kupitia mchakato wa uidhinishaji, pamoja na uchunguzi wa wabunge ambao walithibitisha kufaa kwake kupandishwa cheo hadi katika mahakama ya juu zaidi nchini.

Uteuzi wa Jaji Warsame unajaza nafasi iliyokuwa wazi katika Mahakama hiyo na kuirejesha katika idadi kamili ya majaji kwa mujibu wa katiba kufuatia kifo cha Muhammed Ibrahim Desemba 2025 mmoja wa majaji waliokuwa wakihudumu.

Akiwa mwanasheria mwenye uzoefu mkubwa, jaji Warsame amehudumu katika Mahakama ya Rufaa tangu mwaka 2012, ambapo ameshughulikia kesi muhimu za kikatiba na rufaa.

Kupandishwa kwake kuhudumu katika kiwango cha juu kunatarajiwa kuimarisha mahakama hiyo ambayo hushughulikia kesi nyeti za kikatiba, uchaguzi, na masuala ya maslahi ya umma.

Baada ya kuapishwa, Warsame ataungana na Jaji Mkuu pamoja na majaji wengine katika kutoa maamuzi muhimu katika ngazi ya juu zaidi ya mahakama nchini Kenya.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here