Jaji Mohamed Warsame ameapishwa kuwa jaji wa Mahakama ya Juu nchini Alhamisi tarehe 7 Mei asubuhi katika hafla iliyofanyika ikuluni jijini Nairobi.
Jaji Warsame sasa anaungana na majaji wengine wa mahakama hiyo ya juu zaidi nchini wakiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu pamoja na majaji Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u, Isaac Lenaola na William Ouko.
Wakati wa hafla ya kuapishwa, rais William Ruto alimhimiza Warsame kuendelea kuhifadhi hadhi na urithi wa taasisi ya Mahakama ya upeo, kuchangia maendeleo ya sheria za mahakama hiyo na kuimarisha msingi wa haki.
“Maadili yako, bidii, hekima na uadilifu vitakuwa na nafasi muhimu katika kuandika sura mpya ya maendeleo ya taasisi hii muhimu na kuimarisha imani ya wananchi kwa utawala wa sheria,” alisema rais.
Rais Ruto aliieleza zaidi Mahakama ya Juu kama mlinzi mkuu wa katiba na mwamuzi huru wa masuala makubwa ya kisheria na kikatiba nchini Kenya.
“Ninafurahia kuona kuwa katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, mahakama hii imeendelea kutekeleza wajibu wake kwa uthabiti, ikithibitisha ukuu wa katiba, kulinda mamlaka ya wananchi wa Kenya na kutetea uhuru wa mahakama,” alisema.
Mnamo tarehe 6 Mei 2026, rais Ruto alimteua Jaji Warsame kupitia notisi ya gazeti ramsi la serikali kuwa jaji wa mahakama ya juu baada ya kufaulu mchakato wa usaili na uteuzi uliofanywa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).
Jaji Warsame anajaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya kifo cha jaji Mohammed Ibrahim mnamo Desemba 2025.
Hapo awali, alihudumu katika Mahakama ya Rufaa ya Kenya tangu mwaka 2012 baada ya kupandishwa cheo kutoka Mahakama Kuu, ambako alikuwa ameteuliwa mwaka 2003.
Pia amewahi kuhudumu katika vitengo mbalimbali vya Mahakama Kuu ikiwemo Kitengo cha Biashara, Jinai na Mapitio ya Mahakama, akipata uzoefu mkubwa katika masuala mbalimbali ya sheria.









