Naibu inspekta mkuu wa polisi Eliud Lagat amejiondoa ofisini kwa muda.
Hii ni hatua ambayo amechukua ili kupisha uchunguzi unaoendelea kuhusu mauaji ya mwalimu na mwanablogu Albert Ojwang’ aliyeaga dunia kwa njia tatanishi akiwa mikononi mwa maafisa wa polisi.
Lagat alitangaza kujiondoa kwake kupitia taarifa aliyoitoa Jumatatu, tarehe 16 Juni 2025 akisema kuwa alikuwa tayari kusaidia katika uchunguzi unaoendelezwa na mamlaka ya kuangazia utendakazi wa maafisa wa polisi (IPOA) iwapo angehitajika kufanya hivyo.
Kadhalika Lagat alieleza kwamba majukumu aliyokuwa akitekeleza kwenye ofisi ya naibu inspekta mkuu wa polisi yatashikiliwa na naibu wake hadi uchunguzi utakapokamilika.
“Leo nimeamua kujiondoa kutoka ofisi ya naibu inspekta mkuu wa polisi ili kutoa nafasi kukamilika kwa uchuguzi.” alisema Lagat.
“Majukumu ya ofisi kuanzia sasa yatatekelezwa na naibu wangu hadi uchunguzi utakapokamilika.” aliongeza Lagat.
Wakati huo huo alituma rambirambi kwa familia ya mwenda zake kufuatia mpendwa wao kufariki dunia akiwa mikononi mwa maafisa wa polisi.
Hatua ya Lagat imejiri kufuatia mashinikizo ya kumtaka ajiuzulu kutoka kwa mashirika mbalimbali ya kiraia, viongozi wa kisiasa na wakenya kwa jumla.
Wa punde alikuwa jaji mkuu mstaafu David Maraga siku ya Jumatatu akishinikiza kukamatwa na kushtakiwa kwake.
Ojwang’ alikuwa amekamatwa na polisi kufuatia ujumbe aliouchapisha mtandaoni uliodaiwa kumharibia jina Lagat kwa kumhusisha na madai ya ufisadi.









