Vituo vyote vya polisi nchini vitawekwa kamera za siri (CCTV) katika muda wa miaka miwili ijayo ili kuboresha uwazi na uwajibikaji.
Hili ni agizo la waziri wa usalama wa ndani ya nchi Kipchumba Murkomen akisisitiza kuwa kamera hizo zitakuwa chini ya uangalizi wa afisa mkuu wa kituo (OCS).
Akitoa taarifa kuhusu mageuzi katika idara ya polisi siku ya Jumatatu Juni tarehe 16 2025, katika jumba la Harambee, waziri Murkomen alisema kuwa serikali itahakikisha usalama wa raia vilevile wa maafisa wa polisi.
“Zaidi tutakuwa tunawasilisha mapendekezo katika bunge ili zibuniwe sheria zitakazozuia kuhitilafiwa kwa kamera hizo,” aliongeza waziri.
Murkomen pia alieleza kuwa rekodi katika kitabu cha matukio (OB) zitafanywa kidijitali ili kuzuia kuhitilafiwa.
Haya yanajiri kufuatia ripoti za kuhitilafiwa kwa kamera za siri kwenye kituo cha polisi cha Central katika lile linaloaminika kuwa jaribio lililokusudiwa kuhitilafiana na ushahidi kwa yaliyomsibu mwalimu na mwanablogu Albert Ojwang’ aliyeaga dunia kwa njia tatanishi mikononi mwa maafisa wa polisi.
Ojwang’ anaripotiwa kukamatwa na maafisa wa polisi nyumbani kwao kaunti ya Homabay kisha kusafirishwa hadi jijini Nairobi na kuzuiliwa katika kituo cha Central ambapo baadaye aliripotiwa kuaga dunia.









