Oparesheni ya kuwasaka waliomuua afisa mmoja wa GSU na kuwajeruhi wengine wawili huko Kapedo wakati wa fumanizi itaendelea mpaka washukiwa watakapopatikana.
Hakikisho hili limetolewa na waziri wa usalama wa ndani Dkt. Fred Matiang’i ambaye ameapa kuwa walinda usalama waliotumwa katika eneo hilo watapiga kambi huko hadi wahalifu hao washikwe.
Dkt. Matiang’i aidha ametaja kuwa baadhi ya viongozi wanafadhili shughuli za kihalifu katika eneo hilo na kusababisha utovu wa usalama akisema vitengo vya usalama viko mbioni kuwanasa.
Waziri Matiang’i amesema haya baada ya kukutana na viongozi kutoka Isiolo, Wajir na Garissa akiwemo gavana Ali Korane kujadili hali ya usalama katika mipaka ya kaunti hizo.
Amesema wanaomiliki silaha kinyume cha sheria katika maeneo hayo watapokonywa silaha hizo katika mojawapo wa hatua zinazowekwa kukabiliana na changamoto za usalama.









