Duncan Oburu Ojwang’ amekataa ofa ya rais William Ruto kuongoza tume ya kitaifa ya kutetea haki za kibinadamu (KNCHR).
Hili limejiri wiki moja baada ya rais Ruto kumpendekeza kuwa mwenyekiti wa tume hiyo tarehe 5 Agosti 2025.
Katika barua yake ya Jumanne tarehe 12 Agosti kwa spika wa bunge la kitaifa Moses Wetangula, Ojwang alihusisha uamuzi wake na sababu za kibinafsi pamoja na mgongano wa kimaslahi.
Kulingana naye hali hiyo ingemfanya ashindwe kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Hata hivyo uteuzi wake ulikuwa umepingwa mahakamani na mashirika mbalimbali kwa madai ya ukosefu wa usawa wa kijinsia kwa kuwa naibu mwenyekiti wa tume hiyo alikuwa ni mwanaume.
Uamuzi wake ulipelekea kusitishwa kwa shughuli ya kupigwa kwake msasa iliyokuwa imeratibiwa Jumatano ya tarehe 13 Agosti 2025.
“Kutokana na uamuzi wa Ojwang’ kamati ya sheria na haki inaamuriwa kusitisha mchakato Zaidi wa kumsaili,” Wetangula aliwaambia wabunge.
Ojwang alikuwa miongoni mwa wakenya sita kati ya kumi na saba waliokuwa wamependekezwa kujaza nafasi hiyo mwezi Mei iliyoachwa wazi na Roseline Odede mwenyekiti wa zamani aliyeaga dunia mapema mwaka huu.









