Mwanahabari Robin Njogu amefariki kutokana na matatizo yanayoambatana na virusi vya corona.
Njogu aliyekuwa anafanya kazi na shirika la Royal Media Services alifariki usiku wa kuamkia leo akipokea matibabu katika hospitali ya Agha Khan ambapo alikuwa amelazwa katika kitengo cha watu mahututi ICU.
Njogu amekuwa hospitalini kwa takribani mwezi mmoja sasa.
Akidhibitisha taarifa hizo, waziri wa Habari na Mawasiliano Joe Mucheru amesifia mchangao wa marahemu katika tasnia hii ya unahabari na kutaja kifo chake kama pigo sit u katika sekta hii bali pia kwa familia.
Wanahabari wenza pia wamemwomboleza Njogu na kumtaja kama rafiki wa karibu kwa watu wengi.
Kifo cha Robin kimetokea siku mbili tu baada ya mamake kufariki.
Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wamewaongoza wakenya kumuomboleza mwanahabari Robin Njogu aliyefariki kutokana na matatizo yanayoambatana na corona.
Katika rambirambi zake, Rais Uhuru Kenyatta amesifia mchango wa Njogu katika ukuaji wa radio na sekta ya habari kwa ujumla na kusema mchango wake daima utakumbukwa ikiwemo pia kuwafunza wanahabari wanaoibukia.
Rambirambi sawia na hizo zimetolewa na naibu Rais William Ruto ambaye amemtaja marehemu Njogu kama mwanahabari aliyezingatia sheria za uanahabari na kutaja kifo chake kama pigo kwa taaluma hii.