Vyama tanzu kwenye uliokuwa muungano wa upinzani nchini NASA Amani National Congress ANC, Wiper na Ford Kenya vimetia saini barua rasmi ya kujiondoa kwenye muungano huo.
Katika taarifa ya pamoja iliyosomwa na seneta wa Kakamega Cleophas Malala na mbunge wa Nambale Sakwa Bunyasi, vyama hivyo vimemtaka msajili wa vyama vya kisiasa kufuta muungano huo wa NASA baada ya wenzao wa ODM pia kujiondoa.
Viongozi wa vyama hivyo Musalia Mudavadi wa ANC, Kalonzo Musyoka wa Wiper na Moses Wetangula wa FORD K wametia saini barua hiyo ya kujiondoa NASA wakilalamikia kutokuwepo na uaminifu.
Watatu hao sasa wanasema wako tayari kurindima ngoma ya kuingia ikulu katika uchaguzi mkuu wa Agosti nane hapo mwakani wakitumia muungano wa OKA na kujinadi kuwa na suluhu la matatizo ya wakenya ikiwemo kuwaondolea mzigo wa ushuru.