Wakili Fred Ngatia ameiambia tume ya huduma za mahakama JSC isimnyime kazi ya kuwa Jaji Mkuu kwa sababu ya kuwa wakili rais Uhuru Kenyatta.
Ngatia ambaye aliwakilisha Rais Kenyatta katika kesi za kupinga ushindi wa Urais mwaka 2013 na 2017 amesema alikuwa anatekeleza kazi na kwamba Rais Kenyatta alikuwa na haki ya kuwakilishwa sawia na mkenya mwingine.
Kuhusiana na kesi za uchaguzi wa urais, Ngatia amesema muda wa kisheria wa majuma mawili kwa mahakama ya upeo kutoa uamuzi wa kesi hizo hautoshi.
Licha ya hayo Ngatia anasema iwapo atateuliwa kuwa jaji mkuu na kesi sawia na hiyo kuwasilishwa mbele yake, atafuata sheria kwa kutoa uamuzi kamili kwa muda huo wa siku kumi na nne.
Ngatia pia ameahidi kuhakikisha kuwa kesi zote na haswa zile za uhalifu, zinasikilizwa na kuamuliwa kwa wakati ili kuharakisha zoezi la upatikanaji wa haki.
Wengine ambao watahojiwa ni jaji William Ouko, Profesa Moni Wekesa na Alice Yano.
Wiki iliyopita, watu watano walihojiwa akiwemo wakili Philip Murgor, Jaji David Marete, jaji Martha Koome, msomi Profesa Kameri Mbote na jaji Juma Chitembwe.