Baraza kuu la vyombo vya habari nchini (MCK) limekemea mauji ya mwanahabari wa shirika la KBC Betty Barasa.
Katika taarifa, baraza hilo limehoji kwamba matendo kama hayo dhidi ya waandishi wa habari hayafai na yanakiuka uhuru wa vyombo vya habari.
Kupitia afisa mkuu mtendaji David Omwoyo, MCK limetaka uchunguzi kuhusu mauji hayo kuharakishwa na watuhumiwa kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Mwanahabari huyo aliuawa kwa kupigwa risasi na majambazi akiingia nyumbani kwake Oloolua, Ngong Jumatano usiku.
Inadaiwa wanaume watatu waliojihami na bunduki aina ya AK47 walikuwa wanamsubiri langoni na pindi alipowasili muda wa saa mbili usiku wakamfumania na kuiteka familia yake.
Kisha waliamuru awape pesa na zilipokosa wakamuua kabla ya kutoroka na kipatakalishi na simu mbili za mkononi.
Polisi wameanzisha uchunguzi kuwanasa wakora hao.