Waakilishi wadi wa Nairobi watashiriki uchaguzi siku ya Ijumaa kumtafuta spika mpya baada ya Beatrice Elachi kujiuzulu.
Katika notisi kwenye magazeti ya kila siku nchini, kaimu karani wa bunge hilo Pauline Sarah Akuku amesema wanaotaka kujaza nafasi hiyo wana hadi hapo kesho kutuma maombi yao kwake.
Kwa mujibu wa sheria, spika wa bunge la kaunti hafai kuwa mwakilishi wadi au mfanyikazi mwingine wa serikali.
Wanaotaka kumrithi Elachi pia wametakiwa kuhakikisha kuwa wamesajiliwa kuwa wapiga kura na kuwa wametimiza vigezo vyote vya kisheria ikiwemo maadili.
Kiti hicho kilibakia wazi baada ya Elachi kujiuzulu hapo jana kutokana vurugu ambazo zimekuwa zikikumba City Hall na pia kudai amepokea vitisho.
Wakati uo huo
Gavana wa kaunti ya Nairobi Mike Sonko amewataka waakilishi wadi kukomesha malumbano ya kila mara na badala kuangazia masuala ya maendeleo.
Akizunguzma mapema leo katika kikao na wadau mbalimbali, Sonko amewataka waakilishi wadi kutojigawanya katika mirengo mbalimbali na kusema yuko tayari kuandaa kikao cha kuwaleta pamoja.
Sonko amewataka pia kumuunga mkono mkurugenzi wa shirika la huduma Nairobi NMS jenerali Mohammed Badi kutimiza ajenda ya Rais Uhuru Kenyatta.
Hata hivyo Sonko ambaye jana alilalamikia kuhangaishwa na Badi anataka kuwepo kwa heshima na kufuata sheria katika utendakazi wa shirika hilo.









