Jamii ya Abagusii inaomboleza tena kufuatia kifo cha mbunge wa Bonchari John Oroo Oyioka baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Oyioka alifariki hapo jana, Jumatatu akipokea matibabu katika hospitali ya Aga Khan kaunti ya Kisumu alipolazwa kwa matibabu.
Kifo cha Oyioka kinajiri saa chache baada ya mazishi ya aliyekuwa waziri Simeon Nyachae.
Rais Uhuru Kenyatta, Spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi na kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Amos Kimunya na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ni miongoni mwa viongozi ambao wametuma rambirambi zao kwa familia ya mwendazake.
Katika rambirambi zake, Rais Uhuru Kenyatta amesema marehemu Oyioka ambaye ni mwalimu mstaafu alijitolea kuleta mabadiliko nchini na haswa katika sekta ya Elimu.
Naye spika Muturi amemwomboleza Oyioka akimtaja kama kiongozi aliyejitolea kuhakikisha kuna elimu bora nchini.
Oyioka alihifadhi kiti chake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 kupitia kwa chama cha Peoples Democratic PDP kabla ya kuteuliwa mwanachama wa kamati ya elimu, utafiti na teknolojia.