Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini IEBC imepiga marufuku matumizi ya simu katika vituo vya kupigia kura kikiwamo kituo cha kupigia kura cha Olkalou Julai 16, ikisema watakaopatikana na hatia watatozwa faini ya shilingi milioni moja au kufungwa jela kwa kipindi kisichozidi miaka mitatu.
Akizungumza Jumanne Tarehe 14 Julai 2026, wakati wa kikao cha Pamoja na Idara ya Usalama kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo, Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon amesema kupiga na kusambaza picha za karatasi zao za kura kunakiuka siri ya kura na ni kosa chini ya Kifungu cha 7 cha Sheria ya Makosa ya Uchaguzi.
“Tumeshuhudia baadhi ya watu wakipiga picha karatasi zao za kura na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii. Tunawakumbusha Wakenya, na hasa wapiga kura wa Ol Kalou, msipige picha ya karatasi yenu ya kura baada ya kuipigia kura. Siri na uadilifu wa kura vinahitaji kura yako ibaki kuwa siri. Mtu yeyote atakayekiuka sheria hii atashtakiwa, na akipatikana na hatia atatozwa faini ya hadi shilingi milioni moja au kufungwa jela kwa muda usiozidi miaka mitatu,” amesema Ethekon.
Ethekon amesema Tume imeidhinisha sajili ya wapiga kura itakayotumika katika uchaguzi huo akisisitiza kuwa IEBC itatumia sajili rasmi pekee na kupuuza madai kuwa sajili hiyo imehitilafiwa.
Aidha, amekanusha taarifa zinazosambaa kwamba wapiga kura wanaweza kufika kwenye vituo vya kupigia kura bila kitambulisho cha taifa au pasipoti, akisema madai hayo yanapotosha.
Kadhalika wagombea na vyama vya kisiasa wametakiwa kuwa na wakala mmoja pekee katika kila kituo cha kupigia kura.
IEBC pia imepiga marufuku watu kuvaa mavazi, beji au alama zinazoonyesha kuunga mkono chama cha kisiasa au mgombea ndani ya vituo vya kupigia kura.
Hata hivyo, Ethekon amewahakikishia wagombea na wapiga kura kuwa mchakato wa kuhesabu na kutangaza matokeo utafanyika kwa uwazi, huku mawakala wakiruhusiwa kupiga picha za fomu rasmi za matokeo baada ya kuhesabiwa kwa kura.
“Tumethibitisha sajili ya wapiga kura itakayotumika katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou, na kwa sasa imebandikwa katika kila kituo cha kupigia kura ili wananchi wa Ol Kalou waweze kukagua na kuthibitisha kuwa majina yao yapo kwenye sajili na kwamba wanastahili kupiga kura katika vituo hivyo,” ameongeza.
Ethekon amesema Tume imejizatiti kuhakikisha kuwa sajili rasmi pekee ya wapiga kura ndiyo itakayotumika katika uchaguzi huo.
“Kama IEBC, tunalichukulia suala la sajili ya wapiga kura kwa uzito mkubwa, na tutahakikisha kuwa sajili halisi pekee ndiyo itakayotumika wakati wa uchaguzi huu,” Ethekon amedokeza.









