Viongozi wa kidini wametakiwa kuhakikisha kwamba kanuni za usalama zilizowekwa kuzuia msambao wa virusi vya corona zinazingatiwa kikamilifu kufuatia kuongezeka kwa maambukizi ya ugonjwa huo nchini.
Baraza la pamoja lililobuniwa kuangazia ufunguzi wa maabadi kufuatia kuongezeka kwa visa vya ugonjwa huo linataka masharti hayo ikiwemo kuvalia barakoa wakati wa ibada, waumini kutokaribiana, kuwe na maeneo ya kunawa mikono na sabuni na ibada kudumu kwa muda wa saa mbili pekee kuzingatia vilivyo.
Na huku msimu wa Pasaka ukikaribia, baraza hilo linaloongozwa na askofu Anthony Muheria limepiga marufuku matembezi ya aina yoyote sawa na mikesha ya maombi usiku.
Wazee pamoja na watu wenye magonjwa mbalimbali wanashauriwa kuendelea kuabudu wakiwa nyumbani na wasihudhurie ibada kwa sababu wako katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo. Viongozi wa kidini wanashauriwa kuwatembelea manyumbani na kuomba nao.
Aidha, baraza hilo limetaka matanga kuhudhuriwa na watu wasiopungua 100 alivyotangaza rais Uhuru Kenyatta.
Wito huu unawadia huku kanisa likiendelea kuomboleza kifo cha pasta Mathew Wambua wa kanisa la Deliverance, Donholm aliyefariki kutokana na matatizo yanayoambatana na corona.