Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, ameonyesha matumaini kwamba maandamano yaliyopangwa kufanyika Juni 25, kwa ajili ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu maandamano ya kizazi cha Gen Z, yatakuwa ya amani na yasiyo ya vurugu.
Akizungumza wakati wa mkutano na kaimu Balozi wa Marekani anayeondoka, Mark Dillard, Wetang’ula amesema kuwa Bunge liko tayari kusikiliza hoja za waandamanaji, mradi maandamano hayo yawe ya nidhamu na utulivu.
“Iwapo maandamano hayo yatakuwa ya amani, basi hakutakuwa na wasiwasi wowote, bunge liko tayari kushughulikia maswala hayo, lakini iwapo maandamano yatageuka na kuwa vurugu, basi bunge halitakuwa na uwezo kuyashughulikia, ila asasi zingine zitaingilia kati, lakini natumai yatakuwa ya amani,” alisema Wetang’ula
Balozi Dillard ametumia fursa hiyo kuelezea wasiwasi wake kuhusu matukio ya hivi karibuni, ikiwemo kifo cha Mwalimu na mwanablogu Albert Ojwang mikononi mwa polisi, pamoja na madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi na vyombo vya usalama.
“Tuko makini kuhusu uwajibikaji, kuhakikisha polisi wanawajibishwa huku tukitarajia makumbusho hayo ya kesho yatakuwa ya amani,” alidokeza balozi Dillard
Katika majibu yake, Spika Wetang’ula amesisitiza imani yake katika jukumu la polisi kulinda maisha na mali ya wananchi, lakini amesisitiza kuwa maafisa waovu wanapaswa kuchukuliwa hatua.









