Lawrence Warunge, mshukiwa mkuu wa mauaji ya jamaa zake wanne pamoja na mfanyikazi katika eneo la Karura, Kiambaa kaunti ya Kiambu ameshtakiwa kwa mashtaka matano ya mauaji.
Akifika mbele ya jaji Mary Kasango kwa njia ya mtandao, Warunge ameshtakiwa kwa kumuua babake Nicholas Warunge, mamake Anne Warunge, kakake Christian Njenga, binamuye Maxwell Njenga pamoja na mfanyikazi wao James Kinyanjui Janauri 5-6, 2021.
Hata hivyo Warunge amekanusha mashtaka dhidi yake.
Mahakama imeamuru azuiliwe katika jela la Industrial Area akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake Mei 11, 2021.
Warunge amekuwa akizuiliwa tangu kukamatwa kwake Januari na ameshtakiwa baada ya uchunguzi wa akili kudhibitisha kwamba yuko timamu kushtakiwa.
Mshukiwa wa pili, Sarah Muthoni ambaye ni mpenzi wake Warunge aliachiliwa huru kwa dhamana na atakuwa shahidi wa upande wa mashtaka.









