Jaji Njagi ahojiwa kwa wadhifa wa Jaji Mkuu

0

Mahojiano ya kumtafuta Jaji Mkuu mpya yameingia siku yake ya nne huku ikiwa ni zamu ya jaji David Marete Njagi.

Jaji Njagi ameieleza tume ya huduma za mahakama, JSC, kwamba ana azimio la kukabiliana na mrundiko wa kesi kwa muda wa miaka mitatu iwapo atapewa nafasi ya kuwa jaji mkuu.

Hata hivyo Njagi amekuwa na wakati mgumu kuelezea ni kwa nini kulikuwa na mrundiko wa kesi akiwa jaji wa mahakama ya Kericho licha ya kuwa na azimio la kukabiliana na changamoto hiyo.

Aidha jaji Njagi amesema mikakati yake ya kufanikisha azimio hilo ni utumizi wa mfumo wa kidijitali katika kukabiliana na mrundiko wa kesi pamoja na kuongeza idadi ya wafanyakazi wa idara ya mahakama.

Njagi 62, ni mzaliwa wa kaunti ya Tharaka Nithi akiwa na uzoefu wa miaka 35 katika maswala ya sheria. Alikuwa wakili wa serikali katika afisi ya mwanasheria mkuu kwa miaka 17.

Alifanya kazi kama afisa mkuu wa maswala ya kisheria katika tume ya huduma za waalimu (TSC) kati ya mwaka 2003 na 2009.

Njagi aliteuliwa wakili wa mahakama ya kutatua mizozo ya kikazi mwaka 2012 ambapo amehudumu Nairobi, Kericho na Eldoret.

Wengine ambao wamehojiwa kwa wadhifa huo ni; Said Juma Chitembwe, Profesa Patricia Kameri Mbote na Martha Koome Karambu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here