Rais wa Tanzania Dkt. John Joseph Pombe Magufuli amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 61.
Makamu wa rais Samia Suluhu Hassan amedhibitisha kuwa Dkt. Magufuli amefariki dunia katika hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es Salam mwendo wa saa kumi na mbili jioni saa za Afrika Mashariki kutokana na matatizo ya moyo.
Bi. Samia Suluhu amesema kwamba rais Magufuli alianza kuugua mnamo tarehe 14 mwezi Machi na kulazwa katika hospitali hiyo ambapo alifariki.
Magu anavyofahamika na wengi aliyepewa jina la ‘tingatinga’ amefariki baada ya wiki kadhaa za fununu kwamba alikuwa ameambukizwa virusi vya corona.
Magufuli alizua uzushi kutokana na namna alivyoshughulikia janga la kimataifa la corona ambapo Tanzania haijaripoti visa au vifo vitokanavyo na corona tangu mwezi Aprili 2020.
Ni nini kitafanyika katika uongozi wa taifa hilo?
Kulingana na katiba ya Tanzania makamu wa rais wa nchi hiyo Samia Hassan Suluhu ataapishwa kuhudumu kama rais mpya ili kukamilisha muda uliosalia wa muhula wa miaka mitano wa Magufuli ulioanza mwaka jana”.