Hisia zaendelea kutolewa kufuatia kusimamishwa kwa BBI

0

Mahakama ya Rufaa inatazamiwa kuwapatia mawakili kwenye kesi ya BBI uamuzi kamili uliozika mchakato huo.

Mawakili wa wakereketwa wa mchakato huo Ken Ogeto, James Orengo na Otiende Amollo wanatazamiwa kuamua iwapo au la watapinga uamuzi huo katika mahakama ya upeo.

Tayari kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amekubali kushindwa na kutaja kwamba ni wakati wa kusonga mbele.

Wakati uo huo,

Wakereketwa wa marekebesho ya katiba kupitia mchakato wa BBI wamesema watatumia bunge kuafikia azimio lao.

Mbunge wa Tiaty William Kamket amesema wanaangazia mbinu zingine kubadilisha katiba ikiwemo bunge ili kuhakikisha kwamba wamefaulu.

Hayo yakijiri

Kinara wa chama cha ANC Musalia Mudavadi amelaumu kupuuzwa kwa maoni ya baadhi ya wadau kama sababu kuu iliyosababisha kuanguka kwa BBI.

Kwa upande mwingine,

Naibu rais William Ruto anasema ni wakati wa serikali kuendelea na ajenda ya maendeleo kufuatia kuporomoka kwa BBI.

Ruto akihudhuria ibada ya kanisa katika eneo la Mwea kaunti ya Kirinyaga anasema rasilimali zote zinafaa kutumika kutekeleza maendeleo kwa manufaa ya wananchi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Mahakama ya rufaa Ijumaa ilikubaliana na uamuzi wa mahakama kuu uliosimamisha marekebisho ya katiba kupitia mchakato wa BBI.

Idadi kubwa ya majaji wa mahakama hiyo wakiongozwa na rais Daniel Musinga waliridhia uamuzi wa mahakama kuu ulioamuru kwamba mchakato huo ulikiuka katiba kwa kuzingatia vipengee mbalimbali muhimu.

Majaji Patrick Kiage, Francis Tuiyott, Gatembu Kairu na Hannah Okwengu wameamuru kwamba mchakato huo ulianzishwa na Uhuru Kenyatta wanayesema alitumia visivyo mamlaka yake kutaka kubadilisha katiba.

Kilichobainika kwenye uamuzi vile vile ni kuwa Wakenya hawakupata fursa ya kuhusishwa kikamilifu kwenye mchakato huo huku tume ya uchaguzi IEBC ikikosolewa kwa kudhibitisha sahihi za BBI bila kuwa na makamishna wote.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here