Amnesty International lapinga kufungwa kwa kambi za Wakimbizi

0

Huku makataa ya siku 14 yaliyotolewa na serikali ya Kenya kwa shirika la kimataifa la wakimbizi (UNHCR) kutoa mwongozo utakaotumika kufunga kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma yakikamilika Jumatano, shirika la Amnesty International limepinga kufungwa kwa kambi hizo.

Kupitia mkurugenzi mkuu wa shirika hilo tawi la Kenya Irungu Houghton, Amnesty inahoji kwamba sio salama kuwarudisha wakimbizi hao makwao kwa sababu mataifa kama vile Somalia na Ethopia yanashuhudia msukosuko wa kisiasa.

Badala yake shirika hilo linaitaka Kenya kutumia ushawishi wake katika baraza la usalama la Umoja wa mataifa UN kuishinikiza jamii ya kimataifa kuingilia kati na kuisaidia kubeba mzigo wa kutoa hifadhi kwa wakimbizi.

Shirika hilo vile linahoji kwamba hakuna dhibitisho kwamba kambi hizo zinazotoa hifadhi kwa zaidi wakimbizi laki tano ni tishio kwa usalama kati ya mwezi Januari na Aprili mwaka huu wa 2021.

Shirika la UNHCR tayari limepinga kufungwa kwa kambi hizo likisema hatua hiyo itakuwa na madhara makubwa wakati huu ambapo ulimwengu unapambana na janga la kimataifa la corona.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here