Wataalam wanaonya kuwa Kenya itashuhudia wimbi la nne la maambukizi ya virusi vya corona kwa muda wa wiki mbili zijazo.
Wataalam hao kutoka taasisi ya utafiti wa dawa nchini KEMRI wanasema hili linatokana na kusambaa kwa kasi kwa aina mpya ya virusi vya corona kutoka nchini India.
Wataalam hao wanaonya kuwa kaunti za Nyanza, magharibi mwa Kenya, Nairobi na Mombasa ndizo ambazo zitaathirika zaidi na wanataka hatua za haraka kuchukuliwa.
Wanaonya kuwa huenda kukawa na zaidi ya watu 4,300 katika maeneo hayo ambayo watalazwa hospitalini kutokana na corona na wengine 580 kufariki.
Hospitali za Nyanza na Magharibi mwa Kenya ziko hatarini kulemewa na idadi ya juu ya maambukizi na wataalam hao wanapendekeza mikakati mwafaka kuzuia hilo.
Kwa sasa, wagonjwa waliolazwa katika hospitali mbalimbali ni 1,127 huku wengine 5,722 wakishughulikiwa nyumbani.
Kaimu mkurugenzi wa Afya Patrick Amoth amesema wanapitia utafiti huo kuona uwezekano wa taifa kukumbwa na wimbi la nne la corona.
Haya yanajiri huku maambukizi mapya 376 ya ugonjwa wa corona yakidhibitishwa nchini baada ya kupima sampuli 3,831 katika muda wa saa Ishirini na nne zilizopita.
Idadi ya visa vya ugonjwa huo imeongezeka na kufikia 184,537 huku kiwango cha maambukizi kikiwa katika asilimia 9.8%.
Habari njema ni kwamba wagonjwa 910 wamepona katika muda huo na kufikisha idadi hiyo kuwa 126,594, 6 zaidi wakifariki na kufikisha idadi hiyo kuwa 3,640.
Wagonjwa waliolazwa katika hospitali mbalimbali ni 1,127 huku wengine 5,722 wakishughulikiwa nyumbani.