Wanahabari wanane katika kaunti ya Embu wanaendelea kuuguza majeraha baada ya kuchapwa na maafisa wa polisi wakati wakifuatilia kufurushwa kwa wakaazi wanaoishi karibu na bwawa la Kiambere eneo la Makima.
Wanahabari hao wanasema maafisa wa polisi waliwaamrisha kulala chini na kuwachapa viboko licha yao kujitambulisha kuwa wanahabari.
Wanahabari hao wanasema hii si mara ya kwanza kwao kutandikwa na polisi katika kaunti hiyo. Juhudi zao kutaka kupewa fmu za malalamishi aina ya P3 ziliambulia patupu kwani polisi waliwanyima.
Mbunge wa Mbeere Kusini Geoffrey Kingangi alitiwa mbaroni pamoja na wanahabari hao kabla ya kuachiliwa.
Polisi walikuwa wanawafurusha wakaazi hao kwa madai kuwa ardhi hiyo inamilikiwa na halmashauri ya mto Tana na Athi TARDA. Wakaazi hao wameapa kutongatuka wakidai ardhi hiyo ni yao kihalali.