Hii leo (Ijumaa) ni zamu ya wakili Philip Kipchirchir Murgor kuhojiwa na tume ya huduma za mahakama JSC kwa wadhifa wa jaji mkuu.
Wakili Murgor ni mzaliwa wa mwaka 1961 katika kaunti ya Elgeyo Marakwet na ana uzoefu wa miaka 34 katika taaluma ya uanasheria.
Murgor alikuwa wakili wa serikali katika afisi ya mwanasheria mkuu kati ya mwaka 1986 na 1992 na kisha aliteuliwa kuwa mwendesha mkuu wa mashtaka ya umma mwaka 2003.
Wakili Murgor anahojiwa siku moja baada ya jaji David Marete Njagi kufika mbele ya JSC kunadi sera zake ambapo aliahidi kuweka mikakati kabambe kupambana na ufisadi katika idara ya mahakama.
Jaji Njagi, ameieleza JSC kwamba ana azimio la kukabiliana na mrundiko wa kesi kwa muda wa miaka mitatu iwapo atapewa nafasi ya kuwa jaji mkuu .
Aidha jaji Njagi amesema mikakati yake ya kufanikisha azimio hilo ni utumizi wa mfumo wa kidijitali katika kukabiliana na mrundiko wa kesi na kuongeza idadi ya wafanyakazi wa idara ya mahakama.
Wengine ambao wamehojiwa kwa wadhifa huo ni; Said Juma Chitembwe, Profesa Patricia Kameri Mbote na Martha Koome Karambu.