Naibu wa rais Prof. Kithure Kindiki amesisitiza azma yake ya kuendelea kuhudumu katika nafasi hiyo iwapo serikali ya Kenya Kwanza itapata muhula wa pili.
Kindiki, ametetea nia yake alipokuwa akihutubia maafisa wapya wa ngazi ya mashinani wa chama tawala United Democratic Alliance (UDA), kuhusu kuendelea kushikilia wadhifa huo baada ya uchaguzi wa mwaka 2027, akisema hatakuwa mnyonge wa kushindwa kujitetea ili aondolewe.
“Mimi, fireman, na sasa, kwa neema ya Mungu, naibu rais wa Jamhuri ya Kenya. Je, mnafikiri kuna mtu yeyote anayeweza kuniondoa kwenye kiti hiki na kunifukuza?” Kindiki aliuliza.
“Haiwezekani. Nitajitetea mwenyewe. Siwezi kufukuzwa tu; nitajitetea,” aliongeza.
Ingawa Kindiki hakusema wazi iwapo rais William Ruto amempendekeza kuwa mgombea mwenza wake wa 2027, kauli zake zinaashiria kwamba anaichukulia nafasi yake ya sasa kama wadhifa ambao anakusudia kuutetea na kuendelea kuushikilia.
Ni kauli ambayo inajiri wakati ambapo mazingira ya kisiasa kuelekea 2027 yanazidi kubadilika, huku makundi pinzani tayari yakijipanga kwa nafasi zenye ushawishi katika serikali ijayo ikiwamo naibu rais.
Kuondoka serikalini kwa mtangulizi wake, Rigathi Gachagua, kulitoa nafasi kwa Kindiki, ambaye aliteuliwa kuwa naibu wa rais mnamo Oktoba 2024, baada ya bunge la Seneti kupitisha hoja ya kumuondoa madarakani.
Katika mkutano huo, Kindiki amesisitiza kwamba serikali inapaswa kutadhminiwa kwa rekodi yake ya maendeleo na si kwa kauli za kisiasa au mashambulizi binafsi.
“Tutahakikisha kwamba mwakani, tunapokuja kuomba muhula wa pili wa uongozi, tutawasilisha rekodi yetu ya ahadi tulizotekeleza na zile ambazo tutakuwa tumeanza kuzitekeleza,” alisema.
Tamko lake kwamba atatetea nafasi yake linaweka mazingira ya ushindani mkali zaidi kuhusu muundo wa tiketi ya Kenya Kwanza kuelekea uchaguzi mkuu ujao huku uamuzi wa mwisho kuhusu mgombea mwenza ukitegemea hesabu za kisiasa zitakazohusisha washirika wa muungano wa Kenya Kwanza, maslahi ya kikanda na uwiano wa nguvu ndani ya muungano huo.









