Kenya itaimarisha uhusiano wake na Urusi ili kuongeza kiwango cha biashara.
Rais William Ruto alisema biashara kati ya nchi hizo mbili bado iko chini licha ya uwezo mkubwa uliopo.
Alisema nchi hizo mbili zitatia saini mkataba wa kibiashara ambao utaipa biashara msukumo unaohitajika.
Kiongozi wa Nchi alizungumza hayo siku ya Jumatatu katika Ikulu ya Nairobi, alipomkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov.
Viongozi hao wawili walikubaliana juu ya haja ya kulifanyia mageuzi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kulifanya kuwa mwakilishi bora zaidi na kukidhi mahitaji ya karne ya 21.
Rais Ruto alisema Afrika inapaswa kuwakilishwa katika Baraza la Usalama, ambalo ndilo chombo kikuu cha maamuzi cha Umoja wa Mataifa.
“Bara la Afrika linaweza kuleta mezani mawazo muhimu, mapendekezo na uzoefu ambao utaitumikia dunia vyema,” alieleza.
Rais aliashiria kwamba Kenya na Afrika zinategemea marafiki kama Urusi katika kuunda muundo mpya katika Baraza hilo.
Urusi ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Wanachama wengine ni Marekani, Uingereza, Ufaransa na China.
Baraza la Usalama pia lina wanachama 10 wasio wa kudumu waliochaguliwa kwa mihula ya miaka miwili.
Kuhusu vita vinavyoendelea vya Urusi na Ukraine, Rais Ruto alisisitiza msimamo thabiti wa Kenya kuhusu kuheshimu uadilifu wa eneo la nchi zilizo wanachama kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
“Kenya inataka kutatuliwa kwa mzozo huo kwa njia ya heshima kwa pande zote mbili,” alisema.
Bw Lavrov alisifu urafiki wa miaka 60 kati ya nchi yake na Kenya, akisema uhusiano wa Urusi na bara la Afrika umepata kasi mpya baada ya mkutano wa upeo wa viongozi wa Urusi na Afrika mwaka wa 2019.
Alisema ushirikiano wa kisayansi kati ya nchi hizo mbili umekuwa ukiongezeka.
Bw Lavrov alikuwa Nairobi akielekea kwenye mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa BRICs mjini Cape Town, Afrika Kusini.









