MSWADA WA FEDHA WA 2023 NI WA MANUFAA KWA WANANCHI – RAIS RUTO

0
Rais William Ruto amewataka wabunge kuunga mkono Mswada wa Fedha wa 2023.
 Alisema Mswada huo unalenga kutatua changamoto zinazowakabili Wakenya wa kawaida.
Rais pia alibainisha kuwa Mswada huo utachochea uchumi, kubuni nafasi za kazi na kuongeza mapato.
Aliwataka Wabunge kutokubali shinikizo la Upinzani kupiga kura kinyume na maslahi ya wananchi.
 “Wanapinga ajira kwa vijana na Mpango wa Makazi ambao utawapa Wakenya makazi ya heshima na ya bei nafuu,” alisema.
 Alisema hayo siku ya Jumapili wakati wa ibada ya kutoa shukrani kwa Waziri wa Mazingira Soipan Tuya huko Narok.
 Rais alisema Serikali itatekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba ili kupanua fursa za kiuchumi nchini.
 “Mradi wa nyumba utaimarisha ukuaji wa viwanda vya utengenezaji kama vile saruji na chuma, kukuza biashara za vifaa vya ujenzi na kubuni ajira,” alisema.
 Naibu wa Rais Rigathi Gachagua alisema watakaofaidika na Hazina ya Makazi watakuwa watu wa kawaida.
 “Mradi huu utatoa makazi bora kwa watu wa kipato cha chini kwa bei nafuu,” alisema.
 Miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni Mkewe Rais Rachel Ruto, Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula, Magavana, Mawaziri na wabunge kadhaa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here