Serikali imedhamiria kurudisha katika hali nzuri na kuhifadhi maeneo ya chemichemi za maji nchini.
Rais William Ruto alisema juhudi zinafanywa kurejesha, kukarabati na kuhifadhi mandhari yaliyoharibika.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi la 7 la Upandaji Miti wa Kaptagat unaofanyika kila mwaka katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Rais alisema hatua hiyo haiwezi kutenduliwa.
“Katika kipindi cha miaka 10 ijayo, tutakuza angalau miti bilioni 15 na kurejesha hekta milioni 10.6 za misitu iliyoharibiwa na nyanda za malisho.”
Aidha alisema mpango huo utahusisha umma kikamilifu kuanzia ngazi ya chini hadi kwenye Baraza la Mawaziri.
“Ninatoa wito kwa kila Mkenya kupanda angalau miti 30 kila mwaka,” akaeleza Rais Ruto.
Alielezea masikitiko yake kwamba hali ya hewa kali imekuwa ya kawaida zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na mienendo mibaya ya binadamu.
“Katika nchi na eneo letu, misimu ya ukame imeongezeka kwa wingi, nguvu na muda,”
Alimpongeza Katibu Mkuu wa Hazina ya Kitaifa Chris Kiptoo kwa kampeni yake isiyoyumbayumba ya upandaji miti ambayo sasa imeingia mwaka wake wa saba.
“Juhudi hizi za kipekee ndizo tunazozitaka sasa tunapokabiliana na janga la tabianchi ambalo linatishia maisha yetu ya baadaye.”
Aliongeza kuwa Katibu Mkuu huyo ametia bidii zaidi ya wito wake wa kushinikiza kurejeshwa kwa mfumo wa Ikolojia wa Msitu wa Kaptagat.
Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, Mkuu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi, Mawaziri Kipchumba Murkomen (Barabara), Soipan Tuya (Mazingira), Rebecca Miano (Jumuiya ya Afrika Mashariki), Gavana wa Elgeyo Marakwet Wisley Rotich, Makatibu Wakuu kadhaa wakiongozwa na Chris Kiptoo (Hazina ya Kitaifa), Wawakilishi wa Wadi miongoni mwa viongozi wengine walihudhuria hafla hiyo.