Ombi limewasilishwa katika Mahakama la kutaka Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, Tume ya Kitaifa ya Huduma ya Polisi (NPSC) na maafisa wengine wakuu wa usalama wakiwemo manaibu wa Kanja Eliud Lagat na Gilbert Masengeli, DCI Mohammed Amin na Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor kuwajibishwa kuhusu madai ya kushindwa kuchukua hatua kuhusiana na mauaji, utekaji nyara na mashambulizi ya kikatili ya waandamanaji wa amani.
Wakenya watano Sebastian Ochieng Onyango, Janet Mbithe Wambua, Job Omondi, Macharia Mbugua na Michael Okuto, wanadai wakuu wa usalama walipuuza wajibu wao wa kikatiba wa kulinda maisha, kuchunguza dhuluma na kuwawajibisha wahusika.
Ombi hilo, lililowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Milimani, linataka kulipwa fidia kwa waathiriwa wa madai ya ukatili wa polisi wakati wa maandamano ya 2024-2025.
Walalamishi hao pia wanashinikiza kuanzishwa kwa tume ya mahakama ya kuchunguza na kuchapisha ripoti kuhusu kutojulikana waliko kwa baadhi ya waandamanaji, utekaji nyara na ukatili wa polisi tangu 2020.
Aidha wanadai kuwa vyombo vya usalama vilitumia asasi za usalama zilizopangwa kukandamiza maandamano ya amani, na kusababisha waandamanaji kujeruhiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Kupitia kwa wakili Stephen Musili, walalamishi hao wanadai kuwa zaidi ya watu 80 waliuawa na wengine kadhaa kutekwa nyara wakati wa maandamano ya 2024-2025 huku wakidai polisi waliwakamata zaidi ya watu 1,376 kiholela na kuwajeruhi waandamanaji 1,010.









